“Kuna marafiki wa kula,
marafiki wa kucheka, na wachache sana wa kulia nao usiku wa manane. Wengi huvaa
ngozi ya urafiki, lakini ndani wana ajenda zao. Ukweli huu unauma, lakini ni
lazima usemwe.”
Ndoto ya Urafiki wa Kweli:
Tunaota kuhusu urafiki tangu utotoni, wakati tulikuwa tunagawana
pipi za kijiti shuleni au kukimbizana uwanjani bila sababu ya maana. Tuliamini
kuwa urafiki ni upendo wa dhati, kushirikiana kila kitu, na kuwa pamoja
“milele”.
Tunakumbuka tulivyochora majina ya marafiki wetu kwenye daftari na
kuandika: “Best Friend Forever – BFF.”
Lakini kadri tulivyokua, maisha yalitufunza kuwa si kila aliye karibu yako ni
wako kweli.
Kuna Hadija, msichana aliyekuwa na rafiki yake Halima kwa miaka
sita. Walifanya kila kitu pamoja, shopping, ibada, likizo, hata biashara
walifungua pamoja. Siku Hadija alipogundua kuwa yuko kwenye matatizo makubwa ya
kifamilia na kifedha, alimtafuta Halima lakini simu haikupokelewa, ujumbe
haukujibiwa. Mwezi mmoja baadaye, Halima aliweka picha Instagram akiwa safari
na marafiki wapya, akiwa na tabasamu ambalo Hadija hajawahi kuona kwake.
Na huo ni mwanzo tu.
Uso
Mbili wa Urafiki wa Kisasa:
Urafiki wa sasa umekuwa kama biashara isiyo rasmi, watu wanaingia
kwa faida, si kwa upendo. Ni kama unapanda mti ukitarajia kivuli, lakini
unapomaliza, mtu anauchuna matunda na kukukimbia.
Wengi wako kwako kwa
sababu:
· Unawasaidia
kifedha
· Unawapa
ushauri
· Unatoa muda
wako
· Una jina au
ushawishi
· Unawafariji
wanapoumizwa
Lakini siku ukiwa umevunjika, wamechoka, au huna cha kutoa
watatoweka bila majibu.
Unakumbuka ulivyomkopesha rafiki yako pesa kwa haraka, bila
maandishi? Leo akikupita barabarani anageuza uso. Ule uliyeshiriki naye siri
zako, leo anamwambia mwingine akisema, “hata mimi nilijua hajiwezi.”
Ishara za Marafiki Bandia (Red
Flags):
1. Marafiki wa Matukio Tu
Wanakuja kwenye harusi, wanaku-tag kwenye birthday yako, lakini
hawajui unaumwa. Hawajui ulihangaika kutafuta kodi ya nyumba, hawajui ulikosa
mlo siku tatu. Kwao, maisha ni ya juu juu tu.
2. Wanaoshindana Badala ya Kushirikiana
Unapofanikiwa, wananyamaza. Wanashindwa hata kusema “hongera.”
Badala yake, wanajaribu kukuiga au kukukosoa kisiri wakisema, “siyo lazima
kujionyesha sana.”
3. Marafiki wa Siri
Ukisema kitu mbele yao leo, kesho unakisikia kwa watu wengine.
Wanavaa tabasamu, lakini wana mdomo usiofungwa. Ukikaa nao muda mrefu,
unajikuta umejaa hofu si kwa sababu ya woga, bali kwa sababu huna uhakika kama
kesho utavikwa aibu.
4. Wanapenda Kupokea, Hawajui Kutoa
Unapoitwa rafiki, unaitwa mshirika. Lakini wengine wanaona urafiki
kama mto wa kupokea msaada tu. Hawakumbuki hata kukuuliza kama upo salama.
Urafiki wa Kweli Upo – Lakini Ni
Adimu:
Ndiyo. Urafiki wa kweli upo. Unaweza ukachelewa kuuona, lakini
ukipatikana ni kama neema.
Rafiki wa
kweli ni yule anayekukumbuka bila sababu. Anakutumia ujumbe usiku wa manane
kuuliza, “Uko
salama?”
Ni yule anayejua kuwa hucheki, lakini anakaa kimya tu kukusikiliza.
Ni yule anayelipa nauli ili akusindikize hospitali bila kukulalamikia.
Ni yule anayekuombea kimya kimya bila kukwambia, “nimekuombea.”
Namna ya Kutambua na Kulinda
Urafiki wa Kweli:
1.
Angalia Wakati wa
Shida:
Wakati unapoumia au unaposhindwa – angalia nani anabaki.
2.
Tambua Nafsi ya Mtu: Marafiki wa
kweli hawawezi kuwa watu wasio na huruma. Angalia utu, si ustadi wa maneno.
3.
Jifunze Mipaka: Usimruhusu
kila mtu aingie kwenye maisha yako ndani sana. Tafuta waliothibitishwa kwa
vitendo.
4.
Rafiki wa Kweli
Anakuambia Ukweli: Haogopi kukusema ukienda kinyume. Anakujali zaidi kuliko
anavyokupendeleza.
5.
Mshirikishe Mungu: Maombi
huonyesha mengi usiyoyaona kwa macho. Mwombe Mungu akupe watu wa kweli.
Ushauri wa Maisha – Usiishi kwa
Kivuli cha Urafiki Bandia:
Kuna watu wanabaki kwenye maisha yetu kama sumu ya taratibu.
Wanapunguza thamani yetu, wanadhoofisha ndoto zetu, wanapandikiza hofu na
mashaka. Huo si urafiki ni mzigo.
Achilia waliokuumiza, lakini usijisahau tena. Jifunze. Kua. Tazama
upya. Usitafute wengi tafuta wa kweli mmoja, ni bora kuliko kundi la waigizaji.
Watu Wanabadilika Lakini Ukweli Haubadiliki. Urafiki wa kweli hautengenezwi
kwa picha nzuri au maneno matamu. Hutengenezwa kwa wakati, maumivu, msamaha, na
uaminifu. Wengine walikuja kukutumia, lakini wachache walikuja kukusaidia. Siku
ukipata wa pili, mshikilie kwa moyo wote, kwa sababu katika dunia hii yenye
kelele, kupata rafiki wa kweli ni sawa na kupata hazina.
Palubongo tunasema
hivi: “Jipe nafasi
ya kupendwa na watu wa kweli. Usihofie kupoteza marafiki feki, hofu ya kweli ni
kuishi nao bila kujua.”
**Je, nawe una uzoefu wa aina hii? Tueleze kupitia maoni hapa chini
au tuma ujumbe kupitia WhatsApp yetu. Simama nasi – sisi ni sauti yako._ 💬❤️_
Maoni
Chapisha Maoni