Mahusiano
ni nini?
Maisha
ya mwanadamu hapa duniani yanategemea Sana uwepo wa mtu mwingine, na ndio maana
watu husema sisi binadamu tuna tegemeana kwa Nyanja nyingi sana ili kufanikisha
mambo mengi ya kila siku. Mfano:, ninamuhitaji dereva wa daladala kunifikisha
sehemu ninayohitaji kila siku, ninamuhitaji mwalimu ili kunifundisha na kuniongoza
kupata maarifa katika maisha, ninamuhitaji mlinzi ili kuweka mali zangu salama.
Utegemeano huu kati ya mtu na mtu ndio hupelekea kutokea kwa mahusiano.
Mahusiano
ni hali inayotokea pale mtu anapokuwa karibu na mtu mwingine katika muundo fulani,
wakishirikiana na kutegemeana katika mambo mbalimbali, hali hii huleta
ushirikiano wa kiakili, kihisia, na hata kimwili kulingana na uhusiano wao
ulivyo. Mahusiano yanaweza kuwa kati ya
ndugu na ndugu, rafiki kwa rafiki, familia kwa familia, nchi kwa nchi n.k.
Ijapokuwa mara nyingi ukizungumzia neno mahusiano watu wanakimbilia kwenye
mahusiano ya kimapenzi bila kujua kuwa kuna aina nyingi sana za mahusiano
kulingana na sehemu na wakati. Zipo aina kuu nne za mahusiano ambazo ni
mahusiano ya kifamilia, mahusiano ya kirafiki, mahusiano ya kimapenzi, na
mahusiano ya kawaida ya kufahamiaana tu.
Mahusiano
ya kifamilia ni yale ambayo yanatokana na undugu wa damu au kufahamiana kati ya
mtu mmoja na mwingine au familia moja na nyingine. Mfano:, Kama mmezaliwa
wawili katika familia moja basi nyie mtakuwa na mahusiano ya kindugu kwani
mmeunganishwa na damu zenu na ni familia moja. Kama kuna familia mbili tofauti
lakini wapo karibu Kama ndugu basi na wao wanaingia katika uhusiano huu mfano:,
familia ya shayo wana uhusiano na familia ya mwakasege hii inaonesha ni watu
ambao hawaungani kwa damu lakini wanafahamiana kwa muda, wanashirikiana pamoja
na wamekuwa kama ndugu. Huu ni uhusiano wa kawaida ambao mara nyingi watu
wanaweza kuuelewa.
Mahusiano
ya kirafiki ni yale yanayotokana na mtu na mtu kuwa karibu, wakishirikiana
pamoja katika mambo mbalimbali maishani mwao, na ukaribu huo unaweza kuwepo kwasababu
aidha walisoma pamoja, au wamekuwa pamoja tangu utotoni, au wanafanya kazi
pamoja. Uhusiano wa kirafiki hauishii kwa ngazi ya mmoja tu hapana, hata nchi
na nchi zinaweza kuwa marafiki kutokana na historia zao. Mfano:, nchi yetu
Tanzania ina uhusiano wa kirafiki na nchi kama Malawi, Msumbiji n.k ni kutokana
na historia walizonazo pamoja, pia ujilani wao.
Mahusiano
ya kufahamiana tu, haya huja pale unapokuwa na mtu ambaye hamna historia yoyote
pamoja lakini mmefahamiana hivi karibuni kutokana na tukio fulani au aina
yoyote ya mazingira yaliyojitokeza, uhusiano huu ni ule usio wa ndani kwasababu
pande zote mbili hazijuani kwa kina na wala hawashirikiani sana kama kwenye
aina zingine za mahusiano. Mfano:, inaweza kutokea unamfahamu mtu na una namba
yake ya simu lakini hampo karibu sana kama inavyohitajika na pengine
mnawasiliana tu pale inapohitajika kufanya hivyo.
Aina
ya mwisho ni uhusiano wa kimapenzi, huu ni uhusiano baina ya watu wawili (mara
nyingi ni jinsia mbili tofauti) ambao unawaunganisha kihisia, kiakili na
kimwili. Uhusiano huu umebeba hisia kali za kimapenzi yaani kuhisi upendo kwa
mtu kiasi kwamba mtu huyo anatawala mwili na mawazo yote na kuona hata maisha
hayana maana bila uwepo wa mtu huyo. Ni uhusiano ambao kwa mara nyingi ndio
unazungumziwa sana kwani umebeba mambo mengi na ndio wenye nguvu sana.
Mahusiano yote yaliyotajwa hapo juu yana husisha sana akili na hisia za watu
lakini aina hii ya mahusiano yanaongeza kipengele kingine cha kimwili nikimaanisha
pengine hawa wawili wanagusana kimwili na hata kufanya ngono (tendo la ndoa)
kujiridhisha na kukamilisha matamanio yao na uhusiano wao.
Mahusiano
yote yanaweza kuwa chanya au hasi kulingana tuu na vile mahusiano hayo yanavyo
endeshwa. Aina hizi nne za mahusiano ndizo zinaleta aina zingine zote za mahusiano
zinazo julikana huko nje mfano:, mahusiano ya kibiashara yanaweza kutokea aidha
unamfahamu mtu kirafiki, kifamilia, kimapenzi au mmefahamiana tu kawaida kwa
siku moja.
Ili
mahusiano yaweze kusimama na kuonekana yapo hai kuna sheria, matakwa, mipaka ya
kimaamuzi na mitazamo ya pamoja ambayo huwekwa kuhakikisha mahusiano hayo
yanafanikiwa, na kama mambo hayo hayafatwi au kuwekwa kipaumbele basi mahusiano
hayo yatavunjika na itakuwa ngumu kuyaendesha. Pia ninaamini uhusiano wa nchi
yetu na nchi zingine katika jumuiya ya Afrika mashariki pia una sheria na
mipaka ambayo katika hiyo jumuiya hii imesimama. Vivyo hivyo hata uhusiano wa
kimapenzi unafata taratibu zote kama uhusiano mwingine.
Usikose kuungana nami sehemu inayofuata........!
imeandaliwa na mwandishi Samwel Dihigo.
Maoni
Chapisha Maoni