Kuna watu ambao
kila siku wanainua mataifa bila kupanda jukwaani.
Watu wanaojitoa, lakini hawatajwi.
Watu waliojaa majeraha ya ukimya, lakini bado wanatabasamu.
Leo, Palubongo tunakuletea hadithi ya shujaa tuliyemzoea sana kiasi cha kumsahau
Mwalimu wa Shule ya Msingi.
Asubuhi ya Maisha Yake
Ni saa 11 alfajiri, kijiji cha Ng’ongo bado
kimejaa giza. Ukisikiliza kwa makini, utasikia sauti ya sufuria ikigongana na
jiko la mkaa. Mwalimu Rehema, mama wa watoto watatu, anapika uji wa mahindi kwa
haraka kabla hajavaa kitenge chake cha bluu na kusafiri kwa miguu kilomita nne
kwenda kufundisha darasa la pili.
Barabarani, atakutana na maji ya mvua
yaliyotuama, na wakati mwingine mbwa wa mtaani watamtisha. Lakini kila hatua
anayoipiga, anaiona kama sala ya kimya
kwa ndoto za watoto wake wa darasani.
Anapoingia shule saa 1:30 asubuhi, hakuna
chai, hakuna ofisi yenye kiyoyozi, hakuna kompyuta. Lakini kuna ubao, chaki, na
watoto 72 waliokaa kwenye madawati yaliyopasuka, wakimsubiria shujaa wao mnyenyekevu.
Maisha Yake ya Ndani: Aliyejaa
Mapenzi, Lakini Amepasuka
Mwalimu huyu hana nyumba ya serikali, analala
kwenye chumba kimoja chenye paa la bati linalovuja.
Mwezi ukiisha, anabaki na shilingi elfu 20 baada ya mkopo, ada ya watoto, na
michango ya kijiji.
Anaumwa, lakini hawezi kuacha kazi, kwa sababu anajua hakuna atakayechukua
nafasi yake.
Akipata likizo, badala ya kupumzika, anakwenda kulima ili familia yake isikose
chakula.
Lakini hata katikati ya ugumu huo, anajua sauti yake ya kusema “karibu darasani”
ni mwanzo wa mafanikio kwa wengine.
Je, Tumewahi
Kufikiri Hivi...?
- Daktari
anayekuokoa leo, aliwahi kualikwa darasani na mwalimu aliyelala njaa.
- Mwandishi
unayemsoma, aliandika herufi ya kwanza kwa kalamu ya mwalimu maskini.
- Waziri
anayehutubia, alijifunza kusimama mbele ya watu kwa msaada wa mwalimu wa
darasa la tatu.
Bila mwalimu wa
msingi, hakuna mwanasheria, hakuna injinia, hakuna msanii, hakuna taifa.
Lakini Leo
Tunamwita “Wa Kawaida Tu”
Tunapishana naye
sokoni, hatumsalimii.
Anapoinua mkono kuomba msaada kwa jukwaa, tunamwambia, “Elimu yako ya
kufundisha watoto si lolote.”
Tunamcheka anapovaa viatu vilivyozeeka, tusijue alitumia mshahara wake wote
kununua madaftari kwa watoto wa yatima darasani.
Tunaangalia makalio
ya wasanii wa mitandaoni, lakini hatujawahi kusoma mistari ya uchungu moyoni
mwa mwalimu wetu.
Palubongo inakusimamisha kwa dakika 2
Hebu tafakari...
Ungekuwa nani leo kama mwalimu wako wa darasa la pili asingevumilia ugumu wa
maisha ili akufundishe kusoma “Juma anaenda shule”?
Ungeweza kuandika CV yako?
Ungeweza kuelewa habari kwenye simu yako?
Ungeweza kusoma maandiko ya dini?
Leo, tunakwambia:
Huyu ndiye SHUJAA TUNAYEMDHARAU lakini
ndiye anayelipwa kwa kupandikiza nuru ndani ya giza letu.
Hatua moja mbele
- Toa Shukrani.
Mpigie mwalimu wako wa zamani, mwambie “ASANTE”.
- Toa Sauti.
Simama kwa ajili ya walimu. Waambie wanasiasa, wasanii, jamii: Mwalimu
hastahili dharau.
- Toa Kitu.
Kama unaweza, changia shule ya msingi jirani. Kalamu moja inaweza kubeba
kesho ya taifa.
Toa maoni yako chini 👇
Je, ni mwalimu gani aliyekufanya uamini kwamba
unaweza kufika mbali?
Kumbuka jina lake. Kumbuka tabasamu lake. Leo ni siku ya kumshukuru.

Maoni
Chapisha Maoni