Hebu fikiria… uko
kijijini, usiku wa manane. Mwanamke mjamzito analia kwa uchungu wa uzazi.
Hakuna dawa za usingizi, hakuna madaktari wa kisasa, hakuna glovu wala mashine.
Kisha unajua kuwa njia pekee ya kumuokoa ni… chainsaw. Ndio, ile mashine
tunayojua kwa kukata miti. Ilikuwa ni chombo cha uzazi.
Leo tunaiona chainsaw
kama mashine ya wafyeka mashamba, wachoma mkaa au mafundi seremala. Lakini historia
yake ni tofauti kabisa, ni ya kushtua, ya kugusa moyo na ya kutufundisha kuwa
chanzo cha maumivu kinaweza kuwa mlango wa uzima.
Historia Inayoumiza Lakini
Inahitajika Kusimuliwa
Karne ya 18, kabla sayansi haijakomaa, wakati wanawake walikuwa
wakipoteza maisha kwa uzazi mgumu, madaktari walikumbwa na changamoto: mtoto
amekwama, lakini hakuna njia salama ya kumtoa. Upasuaji wa tumbo (C-section)
ulikuwa sawa na hukumu ya kifo. Hivyo walitafuta njia mbadala, njia ya
kumsaidia mama bila kumuua.
Daktari Jean-René Sigault wa Ufaransa alikuja na wazo la
kushangaza: kuchanua mfupa wa nyonga wa mama
mjamzito. Kwa upanga? Hapana. Kwa kitu kingine chenye nguvu,
lakini pia kisicho haribu sana nyama laini. Hapo ndipo alipoibuka na zana ya
minyororo yenye meno madogo, chainsaw ya kwanza duniani.
Katika upasuaji wa kwanza mwaka 1777, mama mmoja aliyepoteza
watoto wanne kwa sababu ya nyonga nyembamba, alifanyiwa operesheni hiyo ya
“symphysiotomy.” Madaktari walikata mfupa wa nyonga wake kwa kutumia kifaa
hicho, na kwa mara ya kwanza, alijifungua salama.
Chainsaw Haikuanza Msituni, Ilianza
Chumbani kwa Mama
Miaka michache baadaye, madaktari kutoka Scotland — John Aitken na
James Jeffray, waliunda toleo lililoendelea la chainsaw kwa ajili ya uzazi.
Kilikuwa kifaa kidogo kilichokuwa na minyororo laini, kilipitishwa nyuma ya
mfupa wa nyonga kwa sindano maalum, kisha mikono ya daktari ilikitumia kukata
mfupa kwa ustadi mkubwa.
Hiki ndicho kifaa kilichosaidia wanawake wengi waliokumbwa na
uzazi mgumu kabla ya ujio wa operesheni salama.
Baadaye, mwaka 1830, Bernhard Heine alikuja na chain osteotome, kifaa
kilichofanana zaidi na chainsaw ya kisasa, chenye meno, na uwezo wa kukata
mfupa kwa haraka bila kuharibu nyama laini.
Kutoka Uzazi Mpaka Misitu: Ubunifu
Hauwezi Kuzuia Njia Yake
Baada ya miaka mingi, watu walitambua kuwa teknolojia hiyo ya
uzazi ingeweza kutumika kwenye kazi ngumu zaidi kukata miti! Andreas Stihl wa Ujerumani alisajili
chainsaw ya kwanza ya umeme kwa kazi ya ukataji miti mwaka 1926. Kisha
akaongeza toleo la gesi.
Lakini ni hadi miaka ya 1950 ndipo chainsaw ya mtu mmoja
ilipozaliwa. Na hapo ndipo kazi ya misitu ikabadilika milele.
Tunachojifunza Kama Waafrika
Katika jamii zetu, kutoka Bagamoyo hadi Bukoba, mama anapojifungua
ni jambo la familia nzima. Ni tukio la imani, la uchungu na la matumaini. Na
sasa tukijua kuwa chainsaw, chombo kinachovuma kama simba wa msituni,
kilitokana na jitihada za kuokoa maisha ya mama, tunahitaji kukaa na kutafakari.
Hiki si kifaa tu cha mafundi au wachoma mkaa. Ni kumbukumbu ya ubinadamu. Ni somo kuwa hata chombo cha kutisha kinaweza kuwa msaada wa uzima.
Hitimisho:
Hekima ya Maumivu, Neema ya Ubunifu
Katika Palubongo, tunasimulia hadithi zisizosimuliwa. Hadithi
kama hizi zinatufundisha kuwa historia si tu maandiko ya zamani, bali ni mwanga
wa sasa. Tunapoiangalia chainsaw leo, tusione tu nguvu ya kukata, tuone upendo ulioficha ndani yake: upendo wa
kumuokoa mama mjamzito.
Na ndio maana tunasema…
Kila kivuli kina mwangaza wake. Hiyo ndiyo Palubongo.

Maoni
Chapisha Maoni