"Nilifikiria
kuwa ifikapo miaka 30 nitakuwa na biashara yangu kubwa, familia yangu, nyumba
yangu ya ndoto… lakini sasa nipo 35, sina chochote. Nimechoka. Najiona
nimechelewa.”
Labda na wewe unajisemea hivi kila siku. Pengine kila jioni unatazama dari
ukijilaumu, ukijilinganisha na wale mliomaliza shule pamoja ambao sasa wana
magari yao, familia zao, au maisha mazuri ambayo wewe bado unayaota tu.
“Nilizaliwa kwenye familia yenye shida, nimesoma kwa shida,
nimesota kwa miaka mingi, na sasa naona miaka inasonga… na bado sijaona hata
mwanga wa ndoto zangu. Yani Nimechelewa sana kufanikiwa!”
Hapana ndugu yangu. Hujachelewa. Bado
hujachelewa kabisa.
Tumekuwa tukijiambia na kujiapiza mambo mengi
sana, Lakini maisha hayana “ratiba ya darasani.” Maisha yana mitihani,
majaribu, magumu, na changamoto zisizotarajiwa. Na kwa bahati mbaya, yanatokea
hasa pale ambapo tulitarajia mwanga.
Wengine wetu tumetoka kwenye familia masikini,
hatukuwa na walimu wa kutufundisha maisha, hatukuwa na mfano wa kuigwa. Wengine
tunaishi kwenye jamii yenye imani potofu ambapo mtu anaambiwa hawezi kufanikiwa
kwa sababu ya ukoo wake, jina lake, historia ya familia, au unaambiwa “Ulikaliwa
na mizimu”, “Familia yenu ni ya watu waliolaaniwa.”
Lakini leo,
nataka nikuambie kwa sauti ya matumaini: HUJACHELEWA.
kuna vijana waliopitia haya haya, na leo wanang'ara. Hapa kuna
mifano hai, ya kwetu Afrika na si hadithi za mbali:
1.
William Kamkwamba – Malawi (alifanikiwa akiwa na
miaka 14)
Aliwahi kuishi kwenye kijiji kisicho na umeme. Alijifunza kutoka
kwenye vitabu vya zamani vya fizikia vilivyotupwa. Akajenga turbine ya upepo kwa kutumia
mabaki ya vyuma na mashine chakavu. Leo, anazunguka dunia kama mhandisi na
mhamasishaji wa sayansi.
2.
Strive Masiyiwa – Zimbabwe
Alilelewa na mama peke yake baada ya baba kufariki. Alishindwa
mara nyingi kuanzisha kampuni ya simu nchini kwake. Serikali ilimkataa mara kwa
mara. Baada ya miaka 5 ya kesi mahakamani, alipata leseni ya kwanza ya simu.
Leo ndiye mwanzilishi wa Econet Wireless, akiwa bilionea na mmoja wa wafadhili
wakubwa Afrika.
3.
Brian Mwenda – Kenya
Kijana ambaye hakuwa na shahada ya sheria lakini aliweza kuwakilisha
watu mahakamani kwa mafanikio makubwa. Hali yake ilitokana na akili, bidii, na
kupenda kujifunza. Wakati wenzake walipata msaada, yeye alipata dharau—lakini
leo anaungwa mkono kimataifa kwa kipaji chake.
Wapo vijana wengi na watu mashuhuri ambao nisingeweza kuwaandika
wote. Hivyo ndugu yangu nataka nikupe moyo kuwa bado HUJACHELEWA.
Mafanikio Hayana Umri Maalum.
Watu wengi waliotokea kuwa mashujaa wa dunia
hii hawakufanikiwa kwa wakati ule
unaodhani ndio "sahihi." Angalia mifano hii:
- Colonel Sanders
alianza KFC akiwa na miaka 65
baada ya kufutwa kazi mara kadhaa.
- Oprah Winfrey
alikumbwa na unyanyasaji wa kingono akiwa mtoto lakini leo ni mmoja wa
wanawake mashuhuri duniani.
- Morgan Freeman
alianza kupata umaarufu akiwa na miaka 52.
- Jack Ma
alikataliwa kazi zaidi ya mara 30 lakini akaja kuanzisha Alibaba,
kampuni kubwa ya e-commerce.
Unaona? Mafanikio hayafuati saa ya mkononi.
Mafanikio huja kwa wakati wake. Na pengine saa yako ya dhahabu inakaribia kuonesha majira yako.
Kwa Nini Nasisitiza kuwa Bado
Hujachelewa?
- Kwa sababu bado una pumzi. Pumzi ni tiketi ya mabadiliko.
- Kwa sababu unajitambua sasa. Kujitambua ni hatua kubwa ya kuelekea
kwenye mafanikio.
- Kwa sababu kila siku mpya ni nafasi mpya.
Waliowahi kufanikiwa si kwa sababu walikuwa bora kuliko wewe, bali
kwa sababu:
1.
Walikubali hali yao lakini
hawakubaki hapo.
2.
Waliamka kila siku
wakijua hakuna atakayewasaidia isipokuwa wao wenyewe.
3.
Walijifunza, hata
kama haikuwa darasani.
4.
Walikubali kupoteza
usingizi, raha, marafiki… ili wafike walipotaka.
Ushauri Kwa Kijana wa Kiafrika Aliyekata
Tamaa:
- Tafuta Maarifa Mpya;
Elimu haina mwisho. Jifunze kitu kipya kila wiki iwe ni kupitia YouTube, vitabu, kozi fupi, au mentor wa karibu. Kila maarifa mapya ni chombo cha ushindi. - Kataa Imani Potofu;
Sio kweli kwamba huwezi kufanikiwa kwa sababu ukoo wako ni maskini. Historia haikufungi, bali inakupa msingi wa kujenga historia mpya. - Toa Jasho, Sio Malalamiko;
Maisha hayambatani na huruma. Kama huna ajira, jiajiri. Kama huna mtaji, tafuta ujuzi. Kama huna msaada, tafuta marafiki wenye maono. - Lenga Fursa, Usilenge Majuto;
Badala ya kuangalia nyuma ulipokosea, angalia mbele unapoweza kwenda. Fursa zipo mitandaoni, kwenye maonyesho, kwenye mazungumzo ya watu, jitokeze, jiwasilishe. - Zunguka na Watu Sahihi;
Marafiki zako ni kama mbolea au sumu. Tafuta wale wanaokutia nguvu, wanaokuambia “inawezekana”, si wale wanaokushusha na kukuambia “tulizana tu maisha ndio haya.” - Omba Lakini Pia Tenda;
Mungu hasaidii wale wanaolala tu. Anasaidia wale wanaojitahidi. Maombi yawe na matendo.
7.
Amua leo; Usiseme
“nitajaribu mwakani.” Mwaka huo huwezi kuuona kama huanzi leo.
Ndiyo, maisha yanaweza kuwa magumu. Ndiyo,
unaweza kuwa umechelewa kwa ratiba zako mwenyewe. Lakini hujachelewa kwa mpango wa Mungu.
Hujachelewa kwa wakati wako wa pekee.
Inawezekana hujasoma chuo kikuu. Inawezekana hukupata A kwenye
matokeo. Labda baba yako ni mlevi, au mama yako alikuacha ukiwa mdogo. Labda
umejaribu kuanzisha biashara mara 4, zote zikafa. Labda marafiki zako wote
wamepata kazi, wameoa, wameolewa… na wewe bado unapanga mpango wa kesho. Kila mtu ana saa yake. Wakati wako utafika.
Endelea kupambana. Endelea kujifunza. Endelea kuamini. Hujachelewa.
Mtu aliyepanda mti mwaka jana, leo anakula matunda. Wewe ukipanda
leo, utakula miaka ijayo. Usikae ukitazama miti
ya watu wengine. Panda yako. Mwagilia yako. Itaota.
Na siku ikifika, utaangalia nyuma na kusema:
"Nilivumilia.
Nilipambana. Na sasa, nimefika. HUJACHELEWA."
Maoni
Chapisha Maoni