Hadithi ya kweli.
Alipoamua kukaa chini na mume wake kwa
mazungumzo ya kawaida ya jioni, hakuwa tayari kabisa kwa yale aliyokuwa karibu
kusikia.
“Mimi nimekuwa nikikulawiti. Nimekuwa
nikikupatia dawa za usingizi na kukurekodi kwa miaka.”
Maneno haya yalikuwa kama radi ya ghafla.
Alikaa kimya, mwili wake ukawa mzito, akili ikishindwa kutafsiri kilichosemwa.
Mume wake aliyasema hayo kana kwamba ni jambo la kawaida tu. Kama mtu
anayesema, "Kesho tutakula wali na maharage, unaweza kununua
parachichi?"
Kwa miaka mingi, nyuma ya mlango wa nyumba
yao, mwanamke huyu aliishi kwenye ndoa yenye unyanyasaji wa kimwili na kiakili.
Mume wake alikuwa na matatizo ya matumizi mabaya ya dawa na mara kwa mara
alikuwa mkorofi na mwenye hasira.
Kulikuwa na nyakati ambazo aliwahi kuamka
usiku na kumkuta mume wake akimfanyia tendo la ndoa bila idhini yake.
Alipomuuliza, alijitetea kwa kusema hakujua alichokuwa anafanya – eti alikuwa
usingizini na ana matatizo ya kiafya.
Kwa mapenzi yake, mwanamke huyu alimsaidia
kutafuta msaada wa kitabibu. Hakujua kuwa alikuwa ameanza kumwekea dawa za
usingizi kwenye chai kila usiku, kwa lengo la kumbaka bila ridhaa yake.
Baada ya kukiri kwake, alimtisha mkewe kwamba
asithubutu kwenda polisi, la sivyo maisha yake yatakwisha. Alibaki kimya. Huyo
alikuwa baba wa watoto wake. Alishindwa kuamini mtu aliyempenda kwa dhati angeweza
kumuumiza kwa namna hiyo.
Lakini muda ulivyoenda, mwili wake ukaanza
kuonyesha dalili za mshtuko. Akapoteza uzito kwa kasi. Akaanza kupata hofu ya
ghafla (panic attacks). Karibu mwaka baada ya kukiriwa, alipata mshtuko mkubwa
na kuamua kumwambia dada yake kila kitu.
Dada yake alimwambia mama yao, na mama akaita
polisi.
Mume wake alikamatwa na kuhojiwa. Lakini baada
ya siku nne, mwanamke huyu aliwataarifu polisi kuwa hakuwa tayari kufungua
mashtaka. Aliwaza kwa huzuni kubwa,“siwezi kumfunga, si kwa ajili yangu tu,
bali pia kwa ajili ya watoto. Baba yao hangeweza tena kuwa mtu waliomjua.”
Hata hivyo, aliamua mume wake asiendelee
kuishi naye tena, na alimfukuza nyumbani. Hapo ndipo alianza kufikiri kwa kina
juu ya yaliyotokea. Baada ya miezi sita, alirudi polisi na kukubali kufungua
kesi rasmi.
Upelelezi ulianza. Askari wa upelelezi
alimsaidia kuelewa kwamba alikuwa ameathirika vibaya – na kwamba alichopitia ni
ubakaji.
Kipande muhimu cha ushahidi kilitoka kwenye
kumbukumbu za daktari wa akili ambaye mume wake alimtembelea kwa fedha zake
binafsi. Katika maelezo yake, alikiri kwamba alikuwa akimweka mkewe dawa za
usingizi ili aweze kushiriki naye tendo la ndoa bila ridhaa yake.
Aidha, alikiri mbele ya watu wa kanisa lao na
wanachama wa kundi la watu waliokuwa wakipambana na uraibu.
Lakini mwanzoni, ofisi ya mashtaka ilikataa
kufungua kesi dhidi ya mume wake. Mwanamke huyu alikatishwa tamaa. “Kama mtu
anayeweza kukiri hadharani bado hashtakiwi, wanawake wengine wana nafasi gani
ya kupata haki?”
Baada ya kukata rufaa, kesi ilifunguliwa na
ikafika mahakamani miaka mitano baada ya kukiriwa kwa mara ya kwanza.
Katika mahakama, mume wake alidai kuwa mke
wake alipenda "kushtuliwa kwa mapenzi" akiwa amefungwa usingizini –
kitu ambacho jaji na mahakama hawakuamini hata kidogo.
Alikutwa na hatia ya ubakaji, kushiriki ngono
kwa kulazimisha, na kutumia dawa kwa nia ovu. Alifungwa miaka 11 jela na kupewa
amri ya kutokaribia familia yake maisha yake yote.
Ndani ya
miaka mitatu baada ya kesi, mwanamke huyu bado alijenga upya maisha yake. Aliathirika
kiafya na kisaikolojia – alipewa matibabu ya msongo wa mawazo na matatizo ya
neva kutokana na mateso aliyopitia.
Mwisho wa Ukimya, Mwanzo wa Uponyaji
Katika jamii ya Kitanzania, ukatili wa kingono
ndani ya ndoa mara nyingi hufichwa chini ya kivuli cha mila, imani, na heshima
ya familia. Lakini ukweli ni kwamba, tendo la ndoa linahitaji ridhaa – kila
wakati, kila mara.
Wanawake wengi wanaishi na maumivu ya kimya.
Hadithi kama hizi ni muhimu kwa sababu zinavunja ukimya huo, zinachochea
mjadala na kuhimiza haki.
Ni wakati wa kusema: imetosha. Ndoa si
leseni ya kudhulumu. Mpenzi si mmiliki wa mwili wako.
Ikiwa wewe au mtu unayemjua anakumbana na
ukatili wa aina hii, tafuta msaada. Ongea. Simama. Massda upo karibu yako.
~palubongo.
Maoni
Chapisha Maoni