Imeandaliwa na Palubongo.
Mnamo tarehe 24 na 25 Aprili, 2025, kituo cha Centre
for Education and Lifelong Learning (CELL) kilicho chini ya Chuo Kikuu cha
Aga Khan, kilifanya warsha (mafunzo) maalum ya kuwajengea uwezo walimu kutoka
shule mbalimbali namna ya kufundisha masomo ya STEM (Sayansi, Teknolojia,
Uhandisi na Hisabati) kwa ufanisi zaidi, kwa kutumia zana bunifu za kidijitali
kama PhET Simulations.
Warsha hiyo iliyofanyika katika kampasi ya Aga
Khan iliyopo Upanga, Dar es Salaam, iliongozwa na Dkt. Esther Kibga, mtaalamu
mahiri wa elimu ya STEM, akisaidiana na wawezeshaji wenzake Bi. Lucy Rweyemamu
na Bi. Rose Iminza. Kwa muda wa siku mbili, walimu walishiriki katika mafunzo
yenye shughuli shirikishi, majadiliano ya kina, na maonyesho ya mbinu mpya za
ufundishaji wa STEM.
Lengo kuu la warsha lilikuwa kuwawezesha
walimu kuzielewa dhana za elimu ya STEM, kuzifasiri katika mazingira halisi ya
darasani, na kuwasaidia wanafunzi wao kupata ujuzi wa karne ya 21 – ujuzi wa
kufikiri kwa kina, kushirikiana, ubunifu, na utatuzi wa matatizo.
Mojawapo ya nyenzo kuu zilizotambulishwa ni PhET
Simulations, programu shirikishi inayowezesha wanafunzi kuelewa dhana tata
za kisayansi kwa njia rahisi, ya kuona na kushirikiana. Warsha hii ilisisitiza
matumizi ya njia hai za ufundishaji zinazochochea udadisi na kuelewa kwa kina.
Baada ya mafunzo, washiriki
walitunukiwa vyeti vya kuthibitisha umahiri wao mpya katika kufundisha STEM kwa
ubunifu na kwa kutumia teknolojia. Blogu ya Palubongo iliweza kufanya
mahojiano na baadhi ya washiriki wa warsha hiyo ili kupata maoni yao kuhusu
mafunzo.
Mmoja wa washiriki, Mwalimu Samwel Dihigo,
alisema:
“Uwezo wa mwezeshaji kuelezea dhana ngumu za STEM kwa hatua rahisi za vitendo pamoja na matumizi ya PhET simulations, vikiambatana na maudhui bora na ushirikiano wa hali ya juu, vimenipa mbinu ambazo naweza kuanza kutumia darasani mara moja ili kufanya STEM kuwa somo linalovutia na linaloeleweka kwa wanafunzi.”
Kwa upande wa mwezeshaji mkuu wa warsha hiyo,
Dkt. Esther Kibga, alishiriki uzoefu wake kwa kusema:
“Kuendesha warsha (mafunzo) ya STEM ilikuwa ni uzoefu wa kipekee na wa kutia moyo. Kama mtaalamu wa STEM, naamini katika nguvu ya ujifunzaji wa vitendo kuamsha udadisi na kuongeza uelewa. Walimu waliokuwa washiriki walikuja na ari kubwa na mawazo mapya. Ilikuwa ni heshima kujadili mbinu za ubunifu za ufundishaji pamoja nao. Kipengele kimojawapo kilichovutia sana ni utambulisho wa PhET simulations, zana shirikishi inayosaidia kufanya dhana ngumu za kisayansi kuwa dhahiri zaidi kwa wanafunzi. Kwa pamoja tulichunguza namna ya kuleta STEM kuwa hai kupitia mifano halisi ya maisha ya kila siku hapa Tanzania.”
Warsha hii imeacha alama ya kudumu kwa walimu
walioshiriki, na kwa hakika ni hatua muhimu katika kuinua kiwango cha elimu ya
STEM nchini.
{warsha - mkutano wa kujifunza jambo}
Maoni
Chapisha Maoni