"Upweke siyo
laana, ni nafasi ya kuongea na nafsi yako kwa sauti ya ndani ambayo ulimwengu
hauwezi kusikia."
Zamani za kale, kabla ya kuwepo kwa magereza,
jamii zilitumia adhabu za moja kwa moja kama kufukuzwa kwenye kijiji, kuchapwa
viboko au hata kuuawa kwa makosa fulani. Lakini takribani miaka 3,000 iliyopita
huko Mesopotamia (leo ni Iraq), ilibuniwa wazo la kwanza la kumtenga mtu kwa muda kama adhabu — gereza. Lengo halikuwa tu kumwadhibu,
bali kumtenga, ili atafakari
makosa yake na ajirekebishe.
Katika karne ya 18, mfumo wa magereza ulianza
kubadilika huko Ulaya na Amerika. Walianza kutumia "solitary
confinement" yaani kumweka mfungwa peke yake kabisa bila kuzungumza na
mtu yeyote kwa muda mrefu. Lengo lilikuwa kumlazimisha akutane na nafsi yake, akae kimya na kufikiri. Wanafikra wa wakati
huo waliamini kuwa ukimya na upweke
vina nguvu ya kumrekebisha mtu, lakini pia waligundua kuwa ndiyo adhabu kali zaidi kisaikolojia.
Leo hii, hata bila kufungwa gerezani, wengi
wetu tunaishi kwa kuogopa sana kuwa
peke yetu. Lakini kwanini? Ni nini hasa kinatufanya tuone kuwa upweke ni
kama kifungo cha roho?
~~~~~~~~~~~
Kulikuwa na kijana mmoja aitwaye Baraka, aliyekulia kijijini kwetu kule
Tanga. Alikuwa na sauti nzuri, akili nyingi, na haikuwa nadra kumsikia
akiendesha michezo ya kuigiza kwenye mikutano ya vijana. Lakini kulikuwa na
jambo moja alilolikwepa kila mara kama ambavyo vijana wengi wanalikwepa, kuwa peke yake.
Alijaza siku zake kwa watu, kelele, miziki,
mahusiano ya haraka, vikao na safari. Hakuwa anaweza kukaa kimya, wala
kufurahia saa moja bila mtu pembeni.
Lakini bahati au mkosi ukamjia, ghafla alipoteza
kazi, mpenzi wake akaondoka, simu zikawa kimya. Marafiki ndugu na hata vijana
wenzie walipunguza kujumuika nae. Ndipo alikutana na mtu aliyekuwa anamkimbia
maisha yote, nafsi yake.
Nafsi yake ndiyo ukweli wake halisi, hauku - mdanganya,
wala haukumpa furaha isiyo ya kweli. Baraka alikuwa na sonona sana kwa muda mrefu
kwasababu tu alikuwa mpweke.
Katika jamii za Kiafrika, mshikamano na
ushirika ni maadili muhimu sana. Mtu anayeishi peke yake huonekana kuwa na
matatizo. Mwanamke asiyeolewa huonewa huruma. Kijana asiye na marafiki anaambiwa
"anatabia mbaya sana," kana kwamba upweke ni laana.
Lakini ukweli ni kwamba: Tunaogopa kuwa peke yetu kwa sababu upweke
hutuonyesha kile tulichojificha nacho.
Upweke unavua kila kisingizio. Hakuna sifa,
hakuna vicheko vya bandia, hakuna likes za mitandaoni, ni wewe na hali yako ya ndani. Hii ndiyo maana
hata jela, sehemu ya kutisha zaidi ni ya pekee yaani kifungo cha upweke.
Siri ya Upweke: Wema wake na Ubaya
wake
Upweke ni kioo kisichosema uongo. Kinaonyesha
sura yako halisi siyo ile ya kamera au ya mitandao. Kinaonyesha hofu zako,
matarajio yako, ndoto ulizoacha, makosa yako ya zamani, na ukimya wako wa
ndani.
Kwa hiyo, si kwamba watu wanaogopa kuwa pekee,
wanaogopa kukutana na nafsi zao.
Lakini Vipi
Kama Upweke ni Zawadi Iliyofichwa?
Historia inaonyesha kuwa watu wengi waliotenda
mambo makubwa walipitia kipindi cha upweke.
- Nelson
Mandela
alikaa miaka 27 gerezani, sehemu kubwa akiwa peke yake. Akiwa huko
alisoma, alitafakari, akaandika barua na kujifunza lugha za Afrikaans
ambayo ilikuwa hatua muhimu ya kuja kupatanisha Afrika Kusini.
- Wangari
Maathai,
mama shupavu kutoka Kenya, alikataliwa, kudhalilishwa na kutengwa. Lakini
aliendelea kupanda miti peke yake hadi dunia ikamtambua.
- Yesu Kristo, alitumia muda mwingi porini akiwa peke yake kabla ya kuanza huduma yake.
Hata nyumbani, Mama Nuru wa kijiji chetu, baada ya kufiwa na mume wake miaka 30
iliyopita, alihisi dunia imemwacha. Lakini upweke wake ukawa nguvu. Alianza
kufuga, kulima mitishamba, sasa watu wanamsaka kwa uponyaji wa asili. Yote
yalitokana na muda aliotumia akiwa mwenyewe
na Mungu.
Madhara ya
Kuogopa Kuwa Peke Yako;
- Kukosa
kujijua na kujitambua
- Kuweka
tegemeo kubwa kwa wengine kisaikolojia
- Kuingia
kwenye mahusiano yasiyo sahihi ili kuepuka upweke
- Kuzama
kwenye kelele za mitandao ya kijamii hadi kupotea kiroho na kiakili
Jinsi ya
Kugeuza Upweke Kuwa Nguvu;
- Tenga muda wa kimya kila siku – japo dakika 10, usikilize moyo wako.
- Andika hisia zako
– kujieleza kunaondoa machungu ya ndani.
- Soma na tafakari
– vitabu ni marafiki wasiohukumu.
- Tembea bila simu
– tafuta mandhari ya asili; mitende, bahari, au mlima, hapo ndipo nafsi
huongea.
- Jenga uhusiano wa kiroho – sala, dua, au kutafakari ni njia ya
kuponya nafsi.
Upweke Siyo Kifungo, Ni Daraja
Upweke unaweza kuwa gereza, lakini kwa mwenye
maarifa, ni daraja la kuelekea kwenye
nuru. Ni wakati wa kukua, kujijua, na kutulia. Kama jamii, tunapaswa
kuwasaidia vijana wetu wasione upweke kama udhaifu bali kama fursa.
Je, wewe umewahi kuogopa kuwa pekee? Au upo katika kipindi cha ukimya kwa
sasa? Ni nini ulichojifunza ukiwa peke yako?
Tuandikie kwenye maoni au tuma ujumbe kupitia WhatsApp ya Palubongo.
"Palubongo
– Tunasikiliza, Tunahisi, Tunaguswa." 🖤
Maoni
Chapisha Maoni