Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga,
amezindua rasmi kituo kikubwa cha kujaza Gesi Asilia iliyoshindikizwa (CNG)
katika jiji la Dar es Salaam, chenye uwezo wa kuhudumia hadi magari 1,200
kwa siku!
Hatua hii ni sehemu ya jitihada za serikali
kupunguza msongamano kwenye vituo vya zamani vya CNG kama vile Ubungo Maziwa,
na kuhamasisha matumizi ya nishati safi hapa nchini.
Kituo hiki kinasimamiwa na Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kina vifaa vya kisasa, kikitarajiwa
kufanya kazi saa 24 kwa siku. Kimewekewa pampu zinazoweza kuhudumia magari manane
kwa wakati mmoja!
Katika uzinduzi huo, pia lilionyeshwa basi la
mfano kutoka kampuni ya UDART (mabasi ya mwendokasi) ambalo linaendeshwa
kwa kutumia gesi asilia — ishara kuwa hata usafiri wa umma unaanza kuingia
kwenye mageuzi haya ya kijani.
Mhe. Kapinga alisema: “Tumekuwa tukipokea malalamiko mengi
kuhusu foleni ndefu kwenye vituo vya gesi kama vile Ubungo Maziwa. Sasa, ahadi
ya serikali ya kupunguza adha hiyo imetimia.”
Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza mageuzi ya sekta ya
nishati kwa maono makubwa na uongozi madhubuti.
Kwa mujibu wa TPDC, kituo hiki ni cha pili
kwa ukubwa barani Afrika na ndicho kikubwa zaidi katika ukanda wa Afrika
Mashariki! Mbali na magari, gesi pia itasambazwa kwa taasisi kama vile
shule, viwanda na hoteli kupitia malori maalum.
Balozi Ombeni Sefue, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, alisema
kuwa shirika linajipanga kuhakikisha gesi asilia inapatikana kwa matumizi
mbalimbali nchini, ili kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli.
“Foleni ndefu kwenye vituo vya gesi zitabaki
historia.”
Naye Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Kilumbe Ng’enda,
alisifia hatua hiyo akisema matumizi ya gesi kwenye magari yanaweza kupunguza
gharama za mafuta kwa zaidi ya asilimia 40 ukilinganisha na petroli au dizeli.
Hatua hii ni sehemu ya ajenda ya kitaifa ya
kuelekea uchumi wa kijani — uchumi unaotegemea nishati safi, nafuu na rafiki
kwa mazingira.
Je, wewe tayari umejiandaa kuhamia kwenye
nishati safi? Tuambie maoni yako hapa chini! π¬π
~palubongo.

Maoni
Chapisha Maoni