Ruka hadi kwenye maudhui makuu

💞 COUPLES THERAPY (TIBA YA MAPENZI KWA WANANDOA): “Tupo pamoja, lakini je bado tunajuana?”

Maswali 26 ya Kimahaba Kusaidia Mioyo Iliyokaribia Kusahau Mapenzi.

Utangulizi: Upendo Huumiza Kimya Kimya… Tiba Huwaponya Waliochoka Kupendwa

Katika kila ndoa, kuna mambo ambayo hayatamkwi, lakini yanahisiwa. Kuna siku moja utamwangalia mwenzi wako na usione tena yule uliyekuwa ukimtamani kwa macho ya kiu na moyo wa shauku. Si kwa sababu hampendani tena, bali kwa sababu maisha yamewabeba mbali na mlipoanzia.

Ndoa si ndoto tamu kila siku. Kuna siku mtacheka hadi machozi yawatoke, lakini pia kuna siku mtalala migongo ikiwa haijaambiana neno. Watu hubadilika. Mioyo huumia. Mazoea huua msisimko wa mapenzi. Na hapo ndipo tiba ya mapenzi inapohitajika. Si kwa sababu upendo umeisha, bali kwa sababu upendo unahitaji kupaliliwa kama maua bustanini.

Ndiyo maana kila baada ya miaka miwili, wanandoa wanapaswa kupiga breki, kuketi kimya, na kuulizana maswali yanayogusa roho, si akili. Maswali ambayo hufungua milango ya mawasiliano, hukumbusha ahadi, huchambua madonda na pia huamsha shauku mpya.

Hii ndiyo TIBA YA MAPENZI, njia ya kipekee ya kurejesha moto, kuboresha mawasiliano, na kujenga msingi wa kudumu wa mahaba.

Kanuni 5 za Love Therapy (Kabla ya Kuingia Moyoni, Elewana Nia)

  1. Kuwa muwazi na mkweli. Hii si fursa ya kujitetea – bali kujieleza.
  2. Jibu kwa maandishi, na kwa hisia. Andika kwa moyo, si kwa kalamu pekee.
  3. Mkishamaliza, badilishaneni majibu. Kabla ya kusoma… chukueni busu la upendo – lile la kunyamazisha dunia.
  4. Soma majibu ya mwenza wako kwa sauti. Hakikisha anasikia uchungu wako, furaha yako, na matarajio yako kupitia sauti yako.
  5. Zungumzieni kila jibu. Pale kwenye maumivu, pigeni magoti ya maelewano. Pale kwenye furaha, shikeni mikono ya shukrani.

💖 Maswali 26 ya Tiba ya Mapenzi: Kila Swali ni Dawa ya Mahusiano

  1. Ni kitu gani kilikufanya ukamchagua mwenza wako, kuwa wako?
  2. Wakati mnavalishana pete, malengo yako ya ndoa yalikuwa yapi?
  3. Ni nini katika ndoa yako hakikupi furaha kwa sasa?
  4. Ni mambo gani yanayokufanya utabasamu ukifikiria ndoa yako?
  5. Ukipewa nafasi ya kuibadilisha ndoa yako, ungefanya nini?
  6. Unahisi namna gani Mungu anahusika au kuheshimiwa katika ndoa yenu?
  7. Unazungumziaje hali yenu ya mawasiliano? Ina ladha gani?
  8. Mnapataje maamuzi kwenye mambo muhimu yenu wawili?
  9. Mnashughulikiaje migogoro yenu? Mnagusana au mnagusanisha hasira?
  10. Elezea hali ya maisha yenu ya kiroho/imani kama wanandoa.
  11. Kuna ndoa nyingine inayowapa hamasa? Kipi kinavutia kutoka kwao?
  12. Changamoto kubwa mnayopitia ni ipi kwa sasa?
  13. Ni kitu gani kimeifanya ndoa yenu isimame mpaka leo?
  14. Ni mapungufu gani umeyaona ndani ya ndoa yenu?
  15. Mnahitaji kufanya nini ili ndoa yenu ipige hatua nyingine ya kimapenzi na uelewano?
  16. Elezea picha ya ndoa ya ndoto zako – ile inayokufanya ukose usingizi wa furaha.
  17. Ni nini mwenza wako anaweza kufanya kuboresha ndoa yenu?
  18. Ni matatizo yapi unayodhani yametokana na makosa yako mwenyewe?
  19. Unadhani Mungu anafanya nini juu ya ndoa yenu sasa hivi?
  20. Ni kikwazo gani huwa kinawarudisha nyuma katika kusuluhisha tofauti zenu?
  21. Ndoa yenu imebadilikaje tangu muoane – nzuri zaidi au imepungua ladha?
  22. Mwenzi wako akikukwaza – huwa unafanya nini?
  23. Unaonaje tendo la ndoa kati yenu wawili?
  24. Unatosheka na tendo la ndoa? Kama hapana, unahitaji nini kifanyike?
  25. Elezea eneo moja linalowasumbua katika ndoa yenu. Tatizo ni nini na suluhisho linaweza kuwa lipi?
  26. Unamuoneshaje mwenza wako upendo na shukrani? (Love language yako ni ipi?)

Mwisho wa Safari, Mwanzo Mpya wa Mapenzi

Kila swali ni mto wa kujitazama ndani ya macho ya mpenzi wako, si kama mama au baba wa watoto wenu, bali kama yule mpenzi aliyekufanya uone dunia ikiwa na rangi mpya. Zoezi hili halihitaji pesa wala zawadi, linahitaji muda, hisia, na ukaribu wa kiroho.

Washa mshumaa, weka muziki wa taratibu, mvaliane kama siku ya kwanza mlipokutana. Andikeni kwa mikono yenu, sobaneni kwa mioyo yenu, na busuaneni kwa ndimi zenu zenye shukrani.

Ndiyo tiba hii.
Ndiyo mapenzi haya.
Ndiyo ndoa hii.
Na bado mna nafasi ya kuifanya kuwa bora zaidi.

Maoni yako ni ya muhimu!
Umeshajaribu tiba ya mapenzi kama hii? Je, ungependa kuipitia na mwenza wako? Tuambie kwenye comment hapa chini, au shiriki makala hii na wapendwa wengine wanaoitafuta nuru ndani ya ndoa zao.

 

 

Maoni