Kulikuwa na usiku
mmoja wa mwezi mpevu, pale wawili walipokuwa wamekaa pembeni ya ziwa,
wakitazama miale ya mwezi ikicheza juu ya maji, na kupishana na upepo wa
taratibu kama sauti ya mapigo ya moyo uliopendwa. Akiwa amemshika mkono wake
kwa upole, mume alimuuliza mke wake mpya:
“Unajua maana ya honeymoon kweli, au
tumeifuata tu kama mila za harusi?”
Mke alitabasamu,
akitikisa kichwa polepole.
“Ninachojua ni kwamba ni wakati wa
mapenzi matupu. Mapumziko ya wapenzi wapya. Si ndiyo?”
Lakini kama angejua undani wa neno hilo honeymoon, angekumbatia historia ya
karne nyingi zilizopita, historia ya kimahaba, tamu kama asali, yenye ladha ya
mafumbo na maumivu kwa wakati mmoja.
Chimbuko la Neno ‘Honeymoon’
Katika zama za kale, huko Ulaya, neno honeymoon lilitokana na maneno mawili:
"honey" (asali) na "moon" (mwezi). Wakati
huo, asali ilikuwa kiungo cha thamani na ishara ya neema. Ilitumika pia
kutengeneza pombe ya asali (mead) ambayo wapenzi wapya walitakiwa kunywa kila
usiku kwa mwezi mzima baada ya ndoa yao, wakiamini kuwa ingeongeza uwezo wa
kuzaa na kuimarisha upendo wao mpya.
Mwezi mmoja wa kwanza baada ya ndoa ulionekana
kuwa kipindi nyeti cha kujifunza tabia za mwenzi wako, kuzoeana kimwili na
kihisia, na kuimarisha uhusiano wa mapema kabla ya changamoto za ndoa kuanza
kuonekana. Ilikuwa ni safari ya mapenzi safi, wakati wa kutunza moto wa kwanza
wa mahaba usizimike haraka.
Kwa mataifa mengine, kama India ya kale,
wapenzi wapya walikuwa wakipelekwa mahali pa faragha na familia ya mume, ili
wajenge uhusiano wa karibu bila bughudha. Wakati ambapo mwanamke alihitaji kuwa
karibu zaidi na mume, baada ya kuachana na familia yake ya kuzaliwa.
Uzuri Halisi wa Honeymoon
Honeymoon haikuwa safari ya kupiga picha za
Instagram au kutafuta hoteli ya kifahari. Ilikuwa ni njia ya kuunganisha mioyo miwili kwa ukaribu wa kipekee, kipindi
cha kuwa karibu zaidi, kuzungumza bila vizingiti, kucheka kwa uhuru, na
kugundua madoa ya roho za wapenzi wawili.
Ni muda wa
kusema:
“Wewe si tu mwenzi wangu wa ndoa, bali ni rafiki yangu wa roho.”
Ni muda wa kugusa
uso wa mpenzi wako polepole, ukitamani kujua kila chembe ya hisia zake, kwa
sababu hakuna presha ya kazi, ya watoto au ya majukumu. Ni wao wawili tu kama
mwezi na asali.
Watu Wanaokosea Siku Hizi
Katika dunia ya leo, honeymoon imegeuzwa kuwa
tu getaway ya kupiga picha, kula chakula cha gharama au kwenda nje ya
nchi. Wengine wanaikimbiza honeymoon kabla hata ya harusi wakiamini ni sehemu
ya “ku-check compatibility,” jambo ambalo halikuwa dhamira ya asili.
Wengine hukopa mamilioni ili waende Maldives,
lakini wanarudi na migogoro wakidhani honeymoon ni kama filamu ya Disney.
Lakini honeymoon ya
kweli haiko kwenye ramani, iko moyoni.
Ni muda wa kujifunza lugha ya upendo ya mwenzi
wako. Kujua anapenda kuguswa wapi, anapenda kusikilizwa vipi, anapenda
kutabasamu kwa sababu gani. Ni wakati wa kujenga msingi wa ndoa yenu ambao hata
mvua za maisha hazitaweza kuubomoa.
Kwa Ndoa Za Kiswahili, Honeymoon Yako Iko
Wapi?
Katika utamaduni wa Kiswahili, tunayo nafasi
nzuri ya kuifanya honeymoon iwe ya maana. Msiangalie kiasi cha pesa, angalieni
kina cha mawasiliano. Hata kama ni kulala kwenye nyumba ya kupanga ya chumba
kimoja ikiwa na upendo, hiyo ni honeymoon ya maana zaidi ya hoteli ya nyota
tano isiyo na ukaribu wa kweli.
Wapenzi wa leo, jifunzeni kujenga hisia, si
mandhari. Honeymoon yako si lazima iwe Zanzibar au Cape Town, inaweza kuwa hata
kwenye kijiji chenu, lakini ikiwa imejaa kicheko, maongezi ya kiroho, na
mapenzi yasiyoisha, basi ni tamu zaidi ya asali.
Mwezi Ukitua, Mapenzi Yasimame
Mtaalam mmoja wa
mahusiano aliwahi kusema:
“Upendo
wa kweli hujengwa, hautokei tu. Kama mwezi unapotea, moyo ubaki na mwangaza wa
imani, si giza.”
Na ndivyo honeymoon inavyopaswa kuwa. Mwanzo wa mwezi mtukufu wa mahaba. Sio
mwisho wa harusi, bali mwanzo wa safari ya wawili. Safari ya kutengeneza dunia
yao ya faragha, ya maneno matamu, vicheko vya usiku, na kumbatio la milele.
~palubongo.
Maoni
Chapisha Maoni